Mbowe: John Pombe Magufuli Anacheza Ngoma ya Chadema...Adai CCM Imemdhibiti Katika Uteuzi wa Baraza la Mawaziri
Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema anafurahi kuona Rais John Magufuli akitekeleza sehemu kubwa ya sera za chama chake na kwamba kazi ya upinzani si kupinga kila kitu, bali kuangalia masilahi mapana ya Taifa.
Mwenyekiti huyo pia amesema “biashara imeisha” kwa Rais John Magufuli baada ya kutoka kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwa kuwa chama hicho kilimdhibiti katika uteuzi wa Baraza la Mawaziri kiasi cha kumfanya arudishe sura zilezile.
Rais ameanza kazi kwa kishindo baada ya kufumua uozo kwenye taasisi mbalimbali za Serikali kama Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku akidhibiti matumizi ya Serikali kwa kubana safari za nje za watumishi wa umma, kuondoa posho za vikao na pia kuanza utekelezaji wa ahadi ya elimu bure.
Mbowe anaona mambo hayo ndiyo ambayo wapinzani wamekuwa wakipigia kelele wakati wote.
Akizungumza kwenye kipindi maalumu cha Kituo cha Televisheni cha Azam juzi, Mbowe alisema hakuna jambo ambalo Rais Magufuli analifanya ambalo kambi ya upinzani haijawahi kulizungumzia.
Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni hoja ya kubana matumizi ya Serikali, kupunguza safari za nje za viongozi na kupunguza idadi ya watumishi wasio wa lazima.
Mambo mengine alisema ni kupunguza sherehe za kitaifa na kuwa na Serikali ndogo. Alisema kwa kiasi kikubwa Rais anatekeleza sera za upinzani ambazo zilikuwa zinapingwa na wabunge wa CCM.
“Kuwa mpinzani haimaanishi kupinga kila jambo linalofanywa na Serikali hata kama jambo lenyewe ni jema. Ni wajibu wetu kama upinzani kuisimamia Serikali ili kuhakikisha kwamba kila analolisema Rais linatekelezwa kwa vitendo,” alisema Mbowe ambaye pia aligombea urais bila mafanikio mwaka 2005.
Mbunge huyo wa Hai aliongeza kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani itaendelea kutimiza wajibu wake wa kusimamia mambo yenye masilahi kwa wananchi na haitaona haya kuikosoa Serikali pale inapotoka kwenye mstari.
Dk Magufuli ameanza urais kwa kufuta safari za nje hadi kwa kibali cha Ikulu, kumuondoa kaimu mkurugenzi mtendaji wa MNH na kuvunja bodi ya hospitali hiyo, kumuondoa kamishna mkuu wa TRA, mkurugenzi mkuu wa Takukuru, mkurugenzi mkuu wa TPA na katibu mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kutokana na udhaifu alioukuta kwenye taasisi zao. Pia, ameanza kutekeleza ahadi ya elimu bure kwa kuagiza walimu wakuu kutolipisha wanafunzi ada kuanzia Januari na kufuta michango ya aina yoyote shuleni.
Pia, ametangaza Baraza la Mawaziri lenye watu 34, kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru, Siku ya Ukimwi na kupongeza wabunge, akielekeza fedha zilizopangwa kwa shughuli hizo kuelekezwa katika kutatua matatizo ya wananchi.
Mbowe pia hakusita kukosoa Baraza la Mawaziri lililotangazwa na Dk Magufuli.
“Hakuna kipya,” alisema Mbowe.
“Sura ni zilezile zilizokuwapo kwenye Serikali iliyopita na baadhi ya mawaziri wanakabiliwa na kashfa.”
Mwenyekiti huyo alitoa mfano mfano wa uteuzi wa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kwamba haukuwa sahihi kwa sababu ndiye aliyeteua bodi ya Bandari ambayo imevunjwa na Rais kutokana na usimamizi mbovu.
Aliongeza kuwa kurudi kwa Profesa Sospeter Muhongo pia si sahihi kwa sababu aliondolewa kwa uamuzi wa Bunge kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alisema Baraza la Mawaziri halina jipya kwa sababu Rais Magufuli alidhibitiwa na Kamati Kuu ya CCM katika kuliunda.
“Rais alifungwa mikono na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi na tangu ametoka Kamati Kuu biashara imeisha,” alisema Mbowe.
Lakini Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimjibu Mbowe kuwa walitegemea kauli kama huyo kutoka kwa mwenyekiti huyo wa Chadema.
“Mwenyekiti wa Chadema angesifia uteuzi wa Baraza la Mawaziri, ningeshangaa sana,” alisema Nape, ambaye ni pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.
“Alichokisema ndicho wengi tulichokitarajia. Maoni ya Mbowe ni ushahidi wa jinsi asivyojua hata Katiba ya nchi inayoeleza mamlaka ya Rais juu ya uteuzi wa Baraza la Mawaziri kuwa haingiliwi na yeyote.
“Namshauri arudi shule kwa kuwa itamsaidia kuelewa kidogo.”